KUFUNGA NA KUOMBA.

Mch.Gasper Madumla – photo of  2018 at Ununio Mbezi beach / Reach Tanzania Bible collage

Kufunga na kuomba ni namna ya kutesa nafsi/mwili kwa kuunyima chakula na kinywaji kwa makusudi kwa sababu ya kuutafuta uso wa Mungu kwa kumaanisha – Zaburi 35:13

Hivyo “kufunga na kuomba” ni ibada yenye nguvu katika roho,mafundisho ya kufunga yanapaswa kufundishwa mara kwa mara ili kusudi kulijenga kanisa lenye nguvu katika maombi. Historia inatuambia katika kusanyiko la Bwana la kale ( kanisa) lilikuwa na ``siku  maalumu ya kufunga”– Yeremia 36:6

Hii maana yake kanisa lazima liweke kipaumbele kufunga na kuomba, kuwe na utaratibu katika jambo hili. Kama kanisa la kale lililokuwa likidumu katika kuomba na “kufunga” kisha likawa na nguvu,ndivyo kanisa la sasa halina budi kufunga na kuomba mara kwa mara,lipokee nguvu . Kwa sababu “kufunga” ni moja ya ngazi njema katika utumishi uliotukuka – 2 Wakorintho 6:5

Mgawanyo wa fundisho hili umezingatia vipengele vifuatavyo ili kusudi kuleta uelewa zaidi; 

  1. Nini maana ya kufunga.?
  2. Kwa nini tunafunga?
  3. Chanzo cha maombi ya kufunga.
  4. Aina za maombi ya kufunga.
  5. Mifano ya watu waliofunga na wakafanikiwa.
  6. Nini faida ya maombi ya kufunga?
  7. Hasara ya kuishi bila maombi ya kufunga.
  8. Ninawezaje kufunga/ ninawezaje kuishi maisha ya kufunga.?

01. Nini hasa maana ya kufunga?

Pamoja na hali ya kuzuia chakula na vinywaji mwilini pia kufunga ni hali ya kujizuia kabisa katika tabia na mienendo mingi ili kusudi muda huo upate kuomba na kulitafakari Neno la Bwana kwa muda mrefu. Imani ni jambo muhimu katika kufunga kwa maana pasipo hiyo,

hata kama mtu atakaa bila kula wala kunywa bado hataesabika kana kwamba amefunga ,bali amekaa na njaa! Hivyo kuzuia chakula,kuomba na kusoma neno ndani ya muda uliopatana na Mungu tafsiri ya hayo yote ni “kufunga”

2. Kwa nini tunafunga?

  • Kwa sababu tunajifunza kwa Yesu. – Yesu naye alifunga ( Mathayo 4:1-2), Ingawa Yesu alifunga siku 40 mchana na usiku,sisi tunaweza kufunga kwa kadiri atuwezeshavyo Roho mtakatifu. Kama kufunga kusingelikuwa na maana basi sidhani kama Yesu angelifunga. Kila alichokifanya Yesu kilikuwa na maana kubwa sana,na ndio maana anasema “ …mjifunze kwangu…” Mathayo 11:29..
  • Ikumbukwe wazi kwamba,Yesu alikuwa mwanadamu 100% na Mungu %,Na anataka kuona kila mfuasi / follower of Christ,anafanya kile alichofanya.
  • Kuna mambo yasiyotoka,mpaka kufunga na kuomba.- Ingawa wapo watu wanaopinga ukweli huu,lakini ndio ukweli halisia,kwamba kuna mambo mengine yanahitaji kujitoa kwako katika kumtafuta Bwana ndio yapatikanike.  Na kuna mengine hayawezekani mpaka utakapotia ufahamu wa kufunga na kuomba“ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]” Mathayo 17:21

Tafsiri halisi ya andiko hili ni kufunga na kuomba kama mchakato mzima wa maisha ya mwanadamu. Hapa hapana maana kwamba ufunge kwa mambo magumu tu,bali ufunge mara kwa mara kwa sababu ni moja ya msingi wa imani yetu.

Neno la Mungu linatutaka tuwe na maombi na mfungo endelevu kama nguzo/msingi wa imani yetu.  Haya mawili “kufunga” na “kuomba” yanakwenda pamoja,ni mapacha.

Kwa maana mtu mwombaji anapaswa awe mfungaji. Yeye aombaye mara kwa mara bila kufunga hapokei majibu yote kwa maana ameacha kufunga kama utaratibu tena mengine hayatoki namna hii bila kufunga nakuomba. Naye vivyo hivyo yeye afungaye pasipo maombi basi funga yake hukosa nguvu kwa sababu hakuomba wakati wa kufunga.

  • Kufunga kulianzia wapi?

Kufunga kulianzia muda mrefu,tangu enzi hizo kabla ya ujio wa Yesu. Wapo baadhi ya waamini waliokuwa wamekaza kwa Bwana wakijua nini hasa maana ya kufunga na kuomba,nao walifunga.

Na tunashuhudia mtokeo ya watu waliofunga. Hata hivyo,hali haikuwa kama ya sasa kwa maana watu walitumia njia ya kufunga pale walioutafuta uso wa Bwana hasa kwa mambo magumu yaliyoshindikanika. Ebu tazama mfano wa watu wa Yuda chini ya Yehoshafati ;

walipoinukiwa na mataifa matatu yenye nguvu ( waliinukiwa na wana wa Moabu,na wana wa Amoni na wana wa Wameuni. Lakini Yehoshafati akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote – 2 Nyakati 20:1-3)

Na mwishoe akina Yehoshafati wakaibuka washindi. Lakini ukichunguza kilichowafanya waibuke washindi wa vita ni ile hali ya kumtafuta Bwana Mungu kwa njia ya kufunga na kuomba.

Katika agano jipya,“ kufunga na kuomba” ni mazoezi ya kujenga misuli ya imani. Kuanzia kwa Yesu mpaka mitume walitumia muda wao kujijenga kwenye misuri ya imani. Ilikuwa ni kuutafuta uso wa Bwana kwa bidii yote. Tunawaona wengi wakifunga lakini waliomba pia katika Jina la Yesu Kristo.

  • Aina za kufunga.

Biblia imeeleza aina tofauti tofauti za kufunga kulingana na wale waliofanikiwa kufunga. Kwa kadri ya msukumo wa Roho mtakatifu,tunaweza kuona kila mmoja alifunga kwa aina yake. Picha hiyo inatufundisha kwamba “suala la kufunga”

si suala la mtu binafsi kwa matakwa yake bali ni suala la “kuongozwa na Roho mtakatifu’‘. Kwa sababu hiyo,basi Roho ndiye mwenye ratiba kamaili ya kufunga na aina ya kufunga.

i) masaa 12 /masaa ya kawaida – siku kadhaa. Nehemia 1:4

Kuanzia muda wa asubuhi hadi jioni ya saa 12 hivi,bila kula wala kunywa- Mfungo huo ni mfungo wa siku. Mfungo huu unaweza“ kuwa wa siku moja”.  Nehemia naye alifunga aina hii ya mfungo,pia aliomba wakati alipokuwa akifunga – Nehemia 1:4. Hatui haswa siku hizi alizofunga Nehemia zilikuwa ni siku ngapi,bali zilikuwa siku kadhaa.

Ni muhimu kuwa na muda wa kuomba na kusoma neno la Mungu wakati ufungapo –  ( Luka 2:36-37). Ikiwa hakuna muda wa maombi na utulivu wa kulisoma neno la Mungu basi ni dhahili mfungo usifanyike kwa sababu utashindwa kujijenga.

ii) Siku tatu za kawaida au tatu kavu – Esta 4:16,Matendo 9:9

Ukiachilia mbali siku tatu za mfungo wa kawaida,lakini pia kuna tatu kavu. “Tatu kavu” ni kujizuia kula na kunywa kwa muda wa siku tatu mlululizo. Kiwango kizuri cha imani kinahitajika cha kuutiisha mwili katika kula na kunywa kwa siku tatu mfululizo.

Ukweli ni kwamba hatufungi ili kumlazimisha Mungu ajibu,HAPANA!!! Bali kwa imani,tunapofunga Mungu hutusaidia akiangalia kiu,na shauku tuliyonayo,akijibu kwa wakati wake. Pia kuna mfungo wa siku saba

iii) Siku nne – Matendo 10:30

Katika biblia ya NKJV inaeleza kuwa maombi ya Kornelio yalikuwa ya mfungo wa siku nne “ So,Cornelius said Four days ago I was fasting until this hour…”

iv) Siku 21. (Danieli 10:2-3),Siku 40 ( Kutoka 34:28,1 Wafalme 19:8)

Biblia pia inataja aina ya mfungo wa mume na mke – 1 Wakorintho 7:5,bila kutaja hasa ni mfungo wa siku ngapi.

  • Swaumu aliyoichagua Bwana (Isaya 58:6-8)

Kuna kufunga tulikokuchagua sisi kwa malengo yetu mbali mbali,hasi kujiimarisha katika imani yetu. Lakini kuna kufunga alikokuchagua BWANA ambako kunamkazo wa mambo yafuatayo

“kufungua vifungo vya uovu,kulegeza kamba za nira,kuwaacha huru walioonewa,kuvunja nira zote,kuwapa chakula wahitaji,kuwajali maskini” na matokeo yake yatakuwa ni “utukufu wa Bwana utakufuata,na kukulinda”.

Huu ndio mtihani sasa! na ndipo hapo penye kukamilisha funga yako,na hatimaye kulindwa na Bwana,tena biblia inasema utukufu wa Bwana utakufuata. Ni sawa na kusema “upako wa Bwana” hautakupungukia,utalindwa!

05.Mifano ya waliofunga;

Yesu kama kielelezo chetu,naye alifunga. Lakini kuna watumishi wengine walifunga kama vile;

  1. Esta. – Esta 4:16
  2. Musa -Kutoka 34:28
  3. Eliya mtishbi-1 Wafalme 19:8
  4. Hana mama yake Samweli. 1 Samweli 1:18
  5. Ana binti fanueli – Luka 2:36-37
  6. Danieli – Danieli 9:3,10:3
  7. Nehemia- Nehemia 1:4
  8. Watu wa Ninawi -Yona 3:5
  9. Paulo mtue –  2 Wakorintho 11:27
  10. Kanisa la kwanza huko Antiokia – Matendo 13:2-3

06. Matokeo ya kufunga;

  1. Kukujengea misuli ya imani.(Luka 4:1-2)
  2. Kutembea kwenye utukufu wa Bwana (Isaya 58:8)
  3. Kuvikwa nguvu za kiroho na upako.
  4. Kuvikwa sila zote za Mungu kwa ajili ya kuzipinga hila zote za shetani.
  5. Ni chanzo cha kupata kusikia na kuona kiroho.

07. Matokeo yanayoweza kukujia kama huna tabia ya kufunga kabisa – Kuwa kimwili sana,kiasi kwamba hata kushindwa kujua mambo ya rohoni

08. Ninawezaje kufunga?

Wapo watu wengi ambao bado hawawezi kufunga. Wengine ni kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao,kwa mfano magonjwa. Lakini wengine hawajawahi kufunga kwa sababu ya imani walizonazo huko mwanzo walikotoka kwenye dini zao,ambapo kulikuwa hakuna kufunga.

Lakini ikiwa mtu hajawahi kufunga,bado hajachelewa kwa maana anaweza akaanza sasa. Na njia pekee ya kufanikiwa kufunga,ni kumwomba Roho mtakatifu akuwezeshe kwa kuitawala njaa. Yeye anaweza,kwa maana ni Yeye Roho wa Mungu aliyewawezesha wote na ndiye huyo huyo atakuwezesha na wewe pia.

Lakini kitu cha pili ni kuanza taratibu kwa masaa machache ya mwanzo,kidogo kidogo huku ukiendelea kuomba. Mazoezi ni muhimu sana.

Hata hivyo,ni vyema ukawasiliana na mchungaji au mtu wa Mungu aliyepo karibu yako,akuongoze. Kumbuka; kufunga kunakuja kwa sababu ya “nia ya ndani” yaani ujiulize,unafunga kwa nia gani,kitu gani kinakusukuma ndani yako? Na je neno la Mungu linasemaje?

  • Kufunga hutembea na Neno.

Ikiwa kama utafunga,ni lazima usome neno la Mungu. Kwa maana Neno litakuongoza kwa kukupa maarifa ya namna gani uombe pia.

La! Kama unafunga bila Neno,ujue kuna mahali utakwama tu,kwa sababu sio taratibu ya kufunga. Yeyote anayefunga na kuomba ni lazima awe msomaji wa Neno na mwenye “kulitafakari Neno”

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja 

Kwa msaada zaidi maombezi na ushauri (+255) 0781 001 002

 What’s app +255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

63 thoughts on “KUFUNGA NA KUOMBA.

    1. Nashukuru mchungaji kwa somo la kufunga na kuomba
      Na siahayo TU
      Mungu wangu akubsriki
      Thx our postor for your services to serve people of scripture s God.
      Infact aside of fasting and prayer through in Holly sprit is not only that big effect impact
      Be blessed so much

      Liked by 1 person

      1. Pastor ahsante saana kwa SoMo zuri kwani umenifungua kunasehemu kumbe nilikuwa wrong Ila kupitia haya mafundisho naanza kupata mwanga Mungubwambunguni akubariki na uendelee kutupa masomo mengine mengi ahsante saana

        Like

  1. Mungu akubariki sana mtumishi wa Mungu, umenifundisha somo mpaka nimesikia raha, na imenikuta kwenye mfungo wa siku saba, kuombea mambo mbalimbali ya familia yangu na maisha yangu pia.

    Asante Yerkes ajili yako.

    Like

    1. Mungu akubariki sana kwa mafundisho mazuri Mtumishi wa Mungu.Mungu akufunulie zaidi yaliyo ndani ya siri ya maombi ya kufunga.Barikiwa sana.

      Like

  2. Abarikiwe Mtumishi wa Mungu kwa kutupatia neno na kutuonesha mwongozo katika ibada zetu za fungu! Mwenyezi Mungu azidi kuiinua huduma yako hii

    Like

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.