NGUVU YA MANENO.

Maneno ya kinywa chako yana nguvu ya kuumba, pia yana nguvu ya kuua,yana nguvu ya kusababisha uzima hata kutokea,pia maneno ya kinywa chako yana nguvu ya kusababisha mauti.  Waweza kujenga pia waweza kubomoa kwa maneno ya kinywa chako,

waweza kumrejeza mtu mmoja aliyepotea dhambini ukamfanya aokoke kwa maneno tu ya kinywa chako,lakini weweza pia kumpoteza mtu mmoja aliyeokoka akayarudia mambo yake ya kale kwa maneno tu ya kinywa chako. Ndani ya ulimi kuna nguvu ya ajabu;

Hivi unajua kinachowaunganisha wawili kuwa kitu kimoja katika ndoa ni “kiapo cha maneno tu”. Kwa maneno watu huungana na kuwa kitu kimoja,na kwa maneno hayo hayo wawili waweza kuatengana,kutegemea ni maneno gani na wapi yametamkiwa,kama yametamkwa katika madhabahu ndio mbaya zaidi kuleta athali!

Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;…” Mithali 18:21a

Hivyo basi kile kinachoweza kuleta mauti au uzima,kupitia maneno ya kinywa chako ni nguvu iliyomo ndani ya hayo maneno. Bila nguvu yasingetokea hayo uliyoyatamka,kila kitu kitokeacho kimebeba nguvu isababishayo kutokea. Maneno yako yamebeba nguvu kubwa sana. kumbe ulimi umepewa uwezo wa kubeba mauti au kubeba uzima.Na unapotoa nadhiri,unafungwa kwa nadhili hiyo kwa maneno ya kinywa chako.

 “ Mtu atakapomwekea BWANA nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake.” Hesabu 30:2.

Hivyo,wengi leo wametegwa kwa maneno ya vinywa vyao,tena wamejikwaa na kukamatwa kwa maneno

Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako,Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,” Mithali 6:2.

Ni vyema usitumie maneno ya kinywa chako ukasema ujinga tena jitahidi kukizuia kinywa chako kwa kuweka lijamu,ili maneno yako yawe machache. Usiwe mwepesi katika kunena;

 “Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache.” Mhubiri 5:2

Leo hii,watu wengi hupenda kuongea sana kuliko kusikia sana na kwa sababu hiyo wanajikwaa sana,wakitumia vinywa vyao kinyume na mapenzi ya Mungu. Unajua,tumepewa mdomo mmoja na masikio mawili kusudi tusikie zaidi ya kunena. Lakini hali leo imekuwa kinyume badala yake,watu huongea zaidi kuliko kusikia,mbaya zaidi maneno mengi huwa si ya kumpa Mungu utukufu

Tujifunze kwa Yesu,Yeye ambaye ndie kielelezo chetu,Bwana Yesu hakuwa muongeaji sana kama jinsi walivyo watumishi wa leo. Maana kuna wakati alikuwa akiulizwa akitegwa hali akijua nia yao hao waandishi na mafarisayo,Majubu ya Bwana Yesu yalikuwa “wewe wasema” muda mwingine alikuwa kimya. 

Hivi;wajua kwamba kunyamaza ni dawa kubwa sana katika maisha yako? Ukilitambua hilo basi,utatumia vizuri kinywa chako. Kuna watu ambao kweli wameokoka,lakini tatizo ni mdomo! Wanaongea hao! Katika maneno kumi moja tu ndio la ukweli,tisa yote ni uongo~hii ni mbaya sana!

Sote twafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu. Ndivyo biblia isemavyo katika (Waebrania 11:3)Biblia inaeleza tena kwenye kitabu cha Zab.33:6 Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika,na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.Maandiko haya yanatuonesha Nguvu ya uumbaji iliyopo ndani ya neno la Mungu kwa pumzi ya kinywa chake.

Kumbe,hata leo neno la Mungu linaumba nasi tumeshirikishwa kuumba. Hivyo wewe pia waweza kuumba. Swali,unaumba nini? Uzima au mauti? Afya au magonjwa? Mimi nakushauri uumbe afya badala ya magonjwa,uzima badala ya mauti. Twaweza kuumba kwa sababu sisi tu miungu.

Mimi nimesema, Ndinyi miungu,Na wana wa Aliye juu, nyote pia.” Zab.82:6

Nilipokuwa elimu ya sekondari kidato cha pili kabla ya kufanya mtihani wa taifa,tukiwa katika maandalizi ya mwisho mwisho,gafla mwalimu wetu mmoja aliingia darasani na kutuuliza “wangapi wana uhakika watafaulu mitihani hii na kuingia form 3 mwakani?” Sote tukanyoosha mikono yetu juu tukiashilia tutafaulu,lakini palikuwepo na mwenzetu mmoja hakunyoosha mkono.

Mwalimu akamuuliza “ Vipi wewe,kwa nini hukunyoosha mkono wako? Huna huakika wa kufaulu? ” yule mwanafunzi akamjibu mwalimu “ mimi sitafaulu kabisa,wala sitaingia form 3 mwakani”  mwalimu kwa kuwa alikuwa ameokoka na alijua kuwa maneno yanaumba,alimwambia “ usiseme hivyo,..”

Tulipofanya mitihani,kweli yule mwenzetu hakufaulu! Nini kilitokea? Huyu kijana aliona kufeli kabla kufeli kwenyewe. Alionakushindwa kabla ya kushindwa! Na ndivyo tulivyo leo,hatuoni kushinda bali tunaona kushindwa! Kumbuka kuna nguvu ya kuumba,ukiumba kufeli utafeli kweli.

Tuangalie katika biblia watu walioona kufeli kabla ya kufeli nao wakafeli kabisaa. Tuwaangalie wale wapelelezi 10 waliotumwa na Musa kwenda kuipeleleza Kanani,kisha wakawaletea taharifa mbaya wana wa Israeli,tunasoma;

Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.” Hesabu 13:32-33

Kataa kukiri kushindwa,kataa kufeli. Kwa maana hizo ni roho za yule mwovu. Cha ajabu leo kuna watu wanakiri ugonjwa na kusema“ huu ndio ugonjwa wangu mimi…” Hivi,ni nani kakwambia huo ndio ugonjwa wako? Kwa nini kumiliki ugonjwa kwa kukubali kwa kinywa chako? Leo kataa kwa jina la Yesu Kristo,nao huo ugonjwa utakuachia,amini hivyo na inawezekana (Marko 9:23)

Ndugu yangu,ulimi ni kiungo kidogo sana lakini kimejawa na mambo makubwa kuliko jinsi kilivyo.

Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.” Yakobo 3:5-6

Yatafakari hayo maneno,utagundua kwamba mara nyingi watu wamejinajisi kwa maneno yao. Kwa sababu kile kimtiacho mtu unajisi si kile kinachoingia mdomoni bali kile kinachomtoka mtu,kwa maana kinachomtoka mtu hutoka moyoni (Mathayo 15:11) Ulimi ni moto, tena ni moto wa kuotea mbali. Tazama leo,vile ulimi unavyoweza kutenganisha watu katika makanisa. Mtu mmoja tu aweza kuvuruga kundi lote kwa sababu ya matumizi mabaya ya ulimi wake.

~Leo hii tunashuhudia ndoa nyingi zikivunjika kwa sababu ya maneno tu,Watu wanafarakana,kwa sababu ya maneno tu,Wakristo wengi tunashindwa kutumia maneno ya vinywa vyetu katika kujenga tunaishia kubomoa na kubomoana. Jiulize ni mara ngapi unatumia kinywa chako kutamka mabaya kuliko mema? Hali ukijua a kwamba maneno yako yanaumba.

  • Waweza kuhepuka yafuatayo;

01. Usitumie maneno ya kinywa chako katika kulaani.

Naye alipenda kulaani, nako kukampata.Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye,” Zab.109:17

Huyu ndugu alipenda kulaani lakini akalaaniwa yeye. Hii inaonesha hakuwa na neno la kubariki ndani yake,watu wa namna hii huitwa “mabalaki” ambao hakuna neno jema ndani yao,bali laana tu. Balaki yule mwana wa Sipori alituma ujumbe kwa Balaamu ili Balaamu aje amlaanie waisraeli (Hesabu 22:6). Lakini maskini! Balaki hakujua kwamba huwezi kumlaani yeye aliyebarikiwa (Hesabu 23:8)

Hata leo,huwezi kumlaani mtu aliebarikiwa. Ukimlaani huyo utalaaniwa wewe (Mwanzo 27:29). Na ndicho kilichomkuta huyu ndugu wa Zab.109:17

Na ndio maana imeandikwa tena;“Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa.” Isaya 54:17a  . Wazazi epukeni kuwatamkia watoto wenu maneno ya laana. Utakuta mzazi anamwambia mwanawe “ tazama we mtoto,kichwa kama samaki” au“ tazama kichwa kama mbwa!” Ha!

Hii ni mbaya sana,kwa maana mtoto anaweza kuwa na tabia za kimbwa mbwa,au akakuwa akafanana na samaki! Badilisha matumizi mabaya ya maneno yako kwa wanao,badala yake tamka baraka kwa watoto wako kila siku.

2.Usitumie kinywa chako katika uongo pamoja na kupanga mabaya.

Uuzuie ulimi wako na mabaya,Na midomo yako na kusema hila.” Zab.34:13“Umependa mabaya kuliko mema,Na uongo kuliko kusema kweli. ” Zab.52:3

Jifunze kunena kweli kila siku. Chukia tabia ya kusema uongo na tabia ya kusengenya.Kumbuka ya kwamba yeyote anayetumia kinywa chake kusema uongo mara kwa mara, ujue basi huyo bado yupo chini ya utawala wa ibilisi kwa kuwa yeye ndio baba wa huo uongo;baba wa huo uongo;

Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” Yoh.8 :44

Uongo ni mbaya kwa maana ndio dhambi ya pekee ituzingayo kwa upesi. 

Siku zote mwana huyafanya yale tu ambayo baba yake huyafanya. Hata Yesu aliyafanya yale tu ambayo amwona Baba anayafanya ( Yoh.5:19). Vivyo hivyo wale wa shetani huyafanya tu ambayo wanayomuona baba yao anayofanya.

03. Usikae barazani pa wenye mizaha.

 “ Heri mtu yule asiyekwendaKatika shauri la wasio haki;Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.” Zab.1:1.

Kataa kushiriki mizaha,ni dhambi kwa maana inakutia unajisi. Usishiriki kabisa mzaha wowote!

Kumbuka jambo hili; 

Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.” Mathayo 12:36-37

Ninawezaje kupona katika eneo hili?

01.Hakikisha unaulinda moyo wako. – Kwa kuwa kile kinachotoka kinywa mwako, huanzia moyoni,basi huna budi kushughulika na moyo kwanza. 

Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.” Luka 6:45

Hivyo basi katika harakati za kuulinda moyo wako,fanya yafuatayo;

(A)Lijaze neno la Kristo Yesu kwa wingi.

Maneno ya mwisho ya Daudi mwana wa Yese.“Roho ya BWANA ilinena ndani yangu,Na neno lake likawa ulimini mwangu.” 2 Samweli 23:2

(B)Toa mwili wako uwe dhabihu kwa Bwana.- Ni ukweli usiopingika kwamba ikiwa utautoamwili wako kwa matumizi ya kazi ya BWANA basi hautakuwa na muda wa kunena mabaya,maana utakuwa ukiiwaza kazi ya Bwana.

Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Warumi 12:1Hivyo basi tumia vyema maneno ya kinywa chako kwa kufunyika baraka kwa wengi.

Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.

Kwa msaada zaidi, ushauri na maombezi (+255) 0781 001 002

What’s app + 255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

15 thoughts on “NGUVU YA MANENO.

      1. Asante kwa neno lilojaa hekima na nguvu ya Mungu.

        Kweli imo nguvu katika matamshi yatokayo katika vinywa vyetu.

        Namuomba Mungu anisaidie katika hili niwe mtu wa kusikia na kuwa na maneno machache

        Asante.

        Like

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.