ROHO MTAKATIFU NA KAZI ZAKE.

Mch.Gasper.

Roho mtakatifu ni nani?

01.Roho mtakatifu ni nafsi halisi ya tatu ya Mungu baba.

Nafsi hii ilihusika katika uumbaji wa mbingu na nchi (Mwanzo 1:1-3).Hapo zamani iliitwa Roho wa Mungu ( Warumi 8:9,Mwanzo 1:2). Au aliitwa Roho wa Bwana. Hapo mwanzo alikuwa akiachiliwa kwa watu wachache haswa wale tu watakaotiwa mafuta wawe wafalme,au manabii(Waonaji) 1 Samweli 16:13.

Nafsi hii ilikuwa hai,tena halisi ikaayo ndani ya wafalme kuwasaidia kutenda kazi zao ipasavyo. Baada ya Yesu kumaliza kazi ulimwenguni,tunamuona Roho wa Mungu sasa akiitwa Roho mtakatifu.

02.Roho mtakatifu ni Mungu wa kweli.

Lazima watu wote wajue ya kwamba Roho mtakatifu ni Mungu wa kweli aliye hai tena halisi.

Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako?

Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Matendo 5:3-4. 

Angalia pia hapa “Basi `Bwana’ ndiye Roho...”  2 Wokorintho 3:17 na Yoh.4:24

Kwa kuwa Roho ni Mungu wa kweli,basi hatunabudi kumuhitaji sana kwenye maisha yetu ya kila siku,tukamuishie Yeye tu kila siku. Yeye ndio kila kitu kwetu. Kitu ambacho hawakukitambua akina Anania na mkewe Safira kwamba Roho mtakatifu ni Mungu wa kweli,walifikiri ni mwanadamu tu hata wakamuambia uongo.

03.Roho mtakatifu ni msaidizi wetu akaaye ndani yetu ( Yoh.14:16).

Yeye ndie msaada wetu katika yote tuyafanyayo.Tazama,kuna nyakati tatu za msingi zinazoelezewa katika biblia. Nyakati ya kwanza ni Mungu akizungumza ana kwa ana na watumishi wake,kipindi hiki kinajulikana kwa jina la kipindi cha adhabu za  papo kwa papo,au kipindi cha sheria.

Hata hivyo wana wa Israeli hawakuziweza sheria ( agano la kale) na wakalivunja -Yeremia 31:31-34. Baada ya hapo kikaja kipindi cha Mungu kuvaa mwili katika neno Yoh.1:1,&14. Hiki ni kipindi cha pili ambapo tunamuona Yesu akipita huko na huko akihubiri habari njema,akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na ibilisi – Matendo 10:38. Na ikiisha kipindi hicho,Yesu akasema 

Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” Yoh.16:7

Kipindi kilichofuata ni kipindi cha Roho mtakatifu,kipindi hiki ndicho kipindi cha mwisho. Ni kipindi cha neema,lakini kwa sababu ni kipindi cha mwisho basi yafaa kila mmoja ampokee Yesu na kumuani kisha ampokee Roho mtakatifu,Yeye ambaye sasa ndio msaidizi wetu wa kweli.

04.Roho mtakatifu ni nguvu hai ya Mungu ikaayo ndani ya waliokoka kwa kumaanisha. 

Nguvu hii haionekaniki kwa macho,bali tunaweza kuitambua kwa kuangalia matokeo yake. Mfano upepo hakuna awezaye kuuona upepo lakini upepo ukivuma tutaona matokeo yake na kugundua ya kwamba kuna nguvu ya upepo. Hivyo nguvu hii ndio ule uwezo ambapo kila mmoja amepewa ahadi ya kuwa nayo.

Ukweli ni kwamba,ukiokoka tu siku ile ile kunafanyika mageuzi kwenye moyo wako. Mageuzi haya uleta raha fulani,uleta ushuhudiaji yaani unajikuta unatamani umwambie mwenzako kwamba umeokoka. Kitendo cha kutamani kumwambia mwenzako ndio ushuhudiaji wenyewe na ndio moja wapo ya kazi ya Roho mtakatifu. Raha ya moyoni ya namna hii,inadhihirisha kwamba kuna kitu  cha tofauti kimeingia ndani yako;Roho mtakatifu hukupa vyote hivi.

KAZI ZA ROHO MTAKATIFU.

Zifuatazo ni baadhi ya kazi za Roho mtakatifu;

01.Kuwahakikishia wenye dhambi hukumu ( Yoh.16:8)

Bila Roho mtakatifu mtu hawezi kuokoka,kwa maana Yeye Roho mtakatifu ndiye anayekutia hatiani kwamba una dhambi,na kutubu kutokana na mahubiri,mafundisho au shuhuda inayotolewa. Mara zote watu wapatapo hatia ya dhambi,mioyo yao inachomwa (Matendo 2:37).

Hata kufikia hatua ya kufanya maamuzi ya kukata shauri,na kuokoka. Lakini chanzo cha yale maumivu moyoni ni Roho mtakatifu anakushuhudia ya kwamba wewe una dhambi,hatimaye anakuongoza utubu na umpokee Yesu awe Bwana na mwokozi wako.

02.Kufundisha kweli yote ya Mungu na kutukumbusha.( Yoh.14:26)

Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”  Katika andiko hili,tunaziona kazi mbili azifanyazo Roho mtakatifu. Kazi ya kwanza ni kufundisha na pili ni kutukumbusha yote. Leo hii,tunafundishwa na Roho mtakatifu habari njema alizozifanya Yesu na watumishi wote. Bila Roho hatuwezi kuzijua wala hatuwezi kuwa na kumbu kumbu ya yote tuliyoagizwa.

03. Kututakasa 

Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.” 1 Wakorintho 6:11

kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.” 1 Petro 1:2

Kutakaswa ni kuoshwa kutoka katika dhambi,au kufanywa safi kutoka dhambini. Roho mtakatifu anakazi hiyo pia,ya kuhakikisha kuondoa dhambi kwa njia ya neno lake. Soma hapa “…Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli;” 2 Wathesalonike 2:13

04.Anatuongoza( Warumi 8:14,Yoh.16:13)

Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.”  Warumi 8:14. – Hivi,unajua sisi hatujui kule tuendako katika maisha yetu ya kila siku? Bali kwa msaada wa Roho mtakatifu tunashikwa mikono tukitembea naye,

na kutuongoza vizuri katika njia ya imani. Angalia mfano huu,kwa Paulo;Roho mtakatifu alimuongoza ni wapi aende na ni wapi asiende kwa maana kuna mahali alipotaka kwenda Paulo,Roho alimzuia.“   Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,” Matendo 16:7. Soma pia  Matendo 20:22-23.

05.Huumba tabia ya tunda la roho.( Wagalatia 5:22-23)

Yale mambo tisa ya tunda la roho,( upendo,furaha,amani,uvumilivu,utu wema,fadhili,uaminifu,upole,kiasi)uletwa na Roho mtakatifu. Mfano,mtu hawezi kuwa na upendo akiwa nje ya Roho mtakatifu kwa maana upendo huu ni ule upendo wa kumpenda Bwana Mungu na kuwapenda wanadamu wenzako,sasa si lahisi kumpenda Mungu nje ya Mungu yaani nje ya Roho wake.

Ikumbukwe kwamba tunda la roho tuliumbiwa na Mungu hapo mwanzo kabisa kwa maana tuliumbwa kwa sura na mfano wake (Mwanzo 1:26). Hivyo mtu anapomgeukia Mungu akiokoka,mojawapo ya kazi ya Roho mtakatifu ni kurejesha tunda la roho ndani yake.

06. Kutusaidia kuomba 

Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, …..” Warumi 8:26.- Kila mtu duniani ana udhaifu wake katika kuomba na sehemu nyingine. Na ukweli ni kwamba hatujui kuomba itupasavyo bila msaada wa Roho mtakatifu. Ni Yeye tu Roho,ndie anayetuwezesha hata kutamka,kupangilia cha kuombea. Hivyo 

07.Hutuombea kwa kuugua. “…, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Warumi 8:26b

Neno hili “kwa kuugua” lina maana ya kwa kushughulikia haja zetu zote. Ukweli ni kwamba hakuna awezaye kutuombea isipokuwa ni Roho mtakatifu tu. Pale tuombapo kwa Mungu baba na kutaraji kupata majibu,ni Yeye Roho ndie msaadizi wetu wakutuelekeza jinsi ya kuomba ipasavyo kusudi majibu ya kweli tuyapate.

08.Kuihuisha miili yetu.

Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.” Warumi 8:11 Soma pia hapa “…Roho huhuisha” 2 Wakorintho 3:6

Neno hili “kuhuhisha” maana yake ni kuipa uzima,kutia nguvu,kufufua. Roho mtakatifu ambaye alimfufua Yesu katika wafu,ndio huyo huyo atakayetufufua sisi katika miili hii ipate kumuelekea Kristo,neno hili halina maana kwamba tutakufa alafu sasa tutafufuliwa miili. Bali lina maana tutafufuliwa/tutafanywa upya hapa hapa duniani tukiwa hai,kwa maana mtu akiwa mbali na Mungu anahesabika amekufa kwa sababu ya dhambi na makosa yake (Waefeso 2:1). Tukimpokea Yeye tunapata uzima /tunahuishwa katika Kristo Yesu.

09.Kutuwezesha kufikia “uwana”

Uwana” ni hatua ya juu ya kumlingana Mungu katika Kristo Yesu. Pale unapookoka unapewa tu uwezo wa kuwa mtoto wa Mungu (Yoh.1:12). Katika lugha ya kiingereze imejitosheleza kuelezea tofauti ya utoto na uwana,imeeleza“ utoto ni child,bali mwana ni son” Hivyo kupewa uwezo wa kuwa mtoto ni hatua ya kwanza,bali ukizidi kukaa magotini pa Bwana Roho mtakatifu anakuwezesha ukafanyike “ mwana” au son.

Tufanyikapo “wana wa Mungu ” tunafanyika kuwa warithi wa Mungu,warithi pamoja na Kristo-Warumi 8:16-17

10.Kutufariji ( Yoh.14:18-19- “ sitawaacha ninyi yatima”)

Bwana Yesu alieleza kuhusu kifo chake na kufufuka kwake,na akajua ile huzuni itakayokuwepo kwa wanafunzi wake. Lakini akawaambia kwamba hamtakaa mayatima bali Roho mtakatifu mtakuwa naye,atabaki ndani yenu akiwafariji wakati wa hofu,wakati wa kupitishwa mahali pagumu,Yeye Roho atawafariji. Hata sasa,hakuna mfariji mwema kama Roho mtakatifu.

11.Hututunza na kutuwezesha kuishi katika usafi wa roho.

Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.” Wagalatia 5:16 angalia tena katika mistari hii;“Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.” Wagalatia 5:17-18

Usafi wa roho ni maisha ya kumpendeza Mungu kwa kila jambo. Neno hili lisemalo kwamba tukienenda kwa Roho wala hatutazitimiza tamaa za mwili,ni sawa na kusema Roho anatusaidia kutozifuatisha tamaa za miili yetu.

12. Kufafanusha neno la Mungu.

Hakuna mtu yeyote mwenye kulielewa neno la Mungu bila kusaidiwa na Roho mtakatifu. Kazi ya kupata mafunuo,kazi ya kuelewa ujumbe kamili katika mafunuo inafanywa na Roho mtakatifu pekee, imeandikwa;“  lakini, kama ilivyoandikwa,Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia,(Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,)

Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.” 1 Wakorintho 2:9-10. Soma pia 

13.Kutufunulia mambo yajayo.( Yoh.16:13-14)

Katika kitabu cha Amosi neno la Mungu linasema;“ Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Amosi 3:7. Kumbuka ya kwamba,Mungu atakayewajulisha manabii wake ndiye huyo huyo Roho mtakatifu mwenye kufanya kazi hiyo.

14.Kutupa nguvu.

Chukulia mfano wa maji yawezayo kuleta nguvu mwilini,fanya kama vile umetoka safari kisha ukaenda kuoga kitu gani utakihisi baada ya kuoga? Ukweli ni kwamba utachangamka na kuwa na nguvu.

Alkadhalika Roho mtakatifu yeye hututia nguvu za rohoni kwa ajili ya kazi yake. Imeandikwa;“  Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Matendo 1:8 soma pia Matendo 2:1-4 ( ubatizo katika Roho mtakatifu)

15.Kutupa karama na kuziwezesha kufanya kazi.

Tafsiri sanifu ya neno karama ni utendaji wa roho mtakatifu ndani ya mwamini. Kila karama imetolewa na Roho mtakatifu naye ndie afanyaye kazi soma 1 Wakorintho 12:4-11. Bila Roho mtakatifu hakuna karama yoyote itakayopatikana wala kufanya kazi.

Kumbuka; unamuhitaji sana huyu Roho mtakatifu katika utumishi/ukristo wako. Kwa maana wewe huwezi kufanya jambo lolote lile pasipo Roho mtakatifu.

Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi ;

usisite kunipigia simu sasa (+255) 0781 001 002

Mch.Gasper Madumla.

What’s app +255 746 446 446

UBARIKIWE.

27 thoughts on “ROHO MTAKATIFU NA KAZI ZAKE.

  1. Shalom Pastor Gasper,Ubarikiwe kwa mafundisho mazuri. Nimefuatilia mafundisho yako juu ya Roho Mtakatifu,yamenibariki sana. Mungu azidi kukupa mafunuo na usaidie kulijenga Kanisa la Mungu

    Ubarikiwe
    Charles Chris

    Like

    1. asante sana mtumishi wa mungu endelea kunifundisha inanijenga sana

      On Tue, Sep 11, 2018 at 11:47 PM MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. wrote:

      > Colnely commented: “Amen nimepata kitu” >

      Like

    1. Being born again is the base and main way to allow the Holly spirit being with an in you. Therefore one way to receive is to be born agan.
      then,after that you should motivate your holly status by the God’s word everyday

      Like

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.