SABATO

Mch.Madumla
Mchungaji Gasper Madumla ( 2013 ,at Jambo Freight Ltd )

`` Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Mwanzo 2:1-2

Uumbaji wa Mungu haukuwa wa kiholela holela tu,bali aliumba kila kitu katika uzuri na kwa utaratibu. Siku ya saba alipomaliza kufanya kazi yake yote alipumzika. “ Kupumzika” kwa Mungu hakuna maana kwamba alichoka,kwa maana Yeye hachoki,wala hazimii,akili zake hazichunguziki- (Isaya 40:28)

“Mungu akaibarikia siku ya saba” kulikuwa na sababu kubwa sana ya kuibarikia siku ya saba. Kwa mujibu wa andiko hilo,tunaweza kuona kwa nini Mungu aliibarikia,kwa maana andiko linatuambia “alimaliza kuifanya kazi yake,akapumzika” ( Kutoka 20:11)

Hivyo tujifunze kuhusu “mapumziko haya” yalikuwa yanamaanisha nini hasa;

  • Sabato

Neno Sabato katika lugha ya Kiebrania lina maana ya “pumziko” . Neno “pumziko” lina maana ya kuacha kufanya kazi / kustarehe. Kwa kuwa Mungu alipumzika siku ya saba,Hivyo sabato ikalenga kwanza watu wapumzike kufanya kazi,pili wawe na muda na Mungu wao aliyewaumba.

Ili kuifanya siku ya saba ieleweke kwa taifa la mfano la Israeli,Mungu aliweka sheria izungumziayo sabato. Sheria iliwataka wasifanye kazi yoyote,wala watumwa wasifanye kazi,wala ngombe bali siku hiyo ni sikukuu ya kupumzika. Mtu,au mfugo uliokiuka ulipata adhabu ya kuuwawa! -(Kutoka 31:14,16)

Kiini cha ibada katika sabato kilikuwa ni “kutoa sadaka” na kuhakikisha mikate mitakatifu inatunzwa vizuri katika hema la kukutania. Ufunuo wa mikate ilikuwa ni “Neno la Mungu” kwamba Waisraeli wanapaswa kukaa kwenye Neno / maelekezo yote waliyoyapokea.

  • Mwaka wa Pumziko

Sabato haikuishia kwenye siku tu,bali kulikuwa na mwaka wa sabato ambao ulikuwa ni mwaka wa mapumziko . Katika mwaka huu,sheria iliwataka waisraeli wote wafanye kazi kwa miaka sita kisha wapumzishe mashamba yao katika mwaka wa saba.

Mungu alibarikia mazao ya mwaka wa sita nao wakakusanya chakula cha kutosha ili mwaka wa saba mashamba yote yaliachwa bila kulimwa. Kwa kufanya hivi kulitoa nafasi ya mashamba kujikusanyia nguvu ya uzalishaji kwa mwaka mzima wa mapumziko kwa sababu ardhi ikipumzishwa inajitengenezea rutuba yake yenyewe / a natural fertilizer

  • Kwa nini pumziko?

Mtu mmoja aliwahi kusema kwamba “ kama hutapumzika basi kazi zitakupumzisha wewe” . Katika kila kazi kuna haja ya kuwa na mapumziko ili kusudi urejee na nguvu mpya. Lakini hata Mungu kupumzika kwake alikuwa akitufundisha kwamba mwili wa kawaida unahitaji kupumzika,kwa maana mapumziko ni dawa! Katika mapumziko hayo,Bwana apewe nafasi.

Kushika sabato kulikuwa si kwa hiyari bali ni sheria ya muhimu sana,ingawa wengi hawakuweza kushika sabato hasa kipindi cha karne ya kwanza kule kwenye kanisa la Antiokia mpaka leo. Kanisa la kwanza lilikuwa na kusanyiko kila siku ya kwanza ya juma,siku aliyofufuka Bwana ambayo leo ni Jumapili ( Matendo 20:7)

Lakini wengine walibakia katika siku ya saba Jumamosi kwa leo. Hivyo kuwa na siku moja ya kupumzika hasa kwa ajili ya Bwana ni sabato hiyo. Historia inatuonesha kwamba kulikuwa na watu kadha wa kadha waliotaka kujua hasa sabato ni siku gani ili waiadhimishe siku

lakini pia kulikuwa na watu ambao hawafungamanishwi na siku bali wao wamejiwekea utaratibu wa siku moja ambayo kwao ni siku ya Bwana,ni sabato yao. Paulo alikutana na itikadi za watu wa namna hii – Warumi 14:5-6,Wakolosai 2:16

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.

Kwa msaada zaidi,ushauri na maombezi (+255) 0781 001 002

What’s app +255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.